TAMWA YAENDELEA KUWANOA WAHAMASISHAJI JAMII PEMBA.


Wahamasishaji
jamii  kisiwani Pemba wametakiwa kutumia fursa za mafunzo waliyopewa  kua mabalozi wazuri ili kuleta mabadiliko na kufikia lengo la uwiano sawa wa 50/50 kwenye ngazi za maamuzi.


Ameyasema hayo Afisa kutoka afisi ya msajili  wa taasisi zisiso za kiserikali NGO’s Sada Aboubakar Khamis  wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wahamasishaji jamii kwa niaba ya mrajisi wa taasisi hiyo.

Amesema kwa vile demokrasia haikumbaguwa mtu katika kushika nafasi za uongozi ni vyema kuepuka mifumo dume na dhana potofu ya kuwa mwanamke hafai kuwa kiongozi.

Alisema wakati umefika kwa wanawake kuwa na msimamo mmoja wa kuhakikisha wanashika nafasi mbalimbali za uongozi ili nao waweze kutowa maoni katika ngazi za maamuzi.

“Wanawake tuamke tusikae nyuma tunapotoka ni mbali ila kwa sasa ni muda wa kutumia fursa zilizopo kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi",alisema

Awali akitoa tathmini ya ufikiwaji wa awamu ya 2 ya mradi wa SWIL Afisa tathmini na ufuatiliaji kutoka chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake @TAMWA_Zanzibar  Mohammed Kahatib  amesema jumla ya watu million moja na laki sita (1,600,000) wanatarajiwa kufikiwa kupitia awamu hii.

“Kwenye watu million moja na laki sita (1,600,000) wanawake ni elfu kumi na tano (15,000), wanaume elfu sita(6000),asasi za kiraiya (150), wasichana kutoka vyuoni na skuli mia sita (600), watu mashuhuri kutoka taasisi tofauti za kiserikali na binafsi mia saba(700)” Alisema.


 Mkufunzi wa mafunzo hayo Fat-hiya Mussa Said amesisitiza kuendelea kuthaminiwa juhudi zilizochukuliwa hapo awali ili kupeleka mbele gurudumu la wanawake na uongozi.

Aliongeza kunahitajika mashirikiano ya pamoja kati ya wahamasishaji jamii  wa zamani na wale  walioingia awamu hii ili malengo yaliyokusudiwa yafanikiwe.

"Mashirikiano yenu ndio yatakayofanikisha lengo hili na kutasaidia wanawake wengi kujitokeza kwenye demokrasia , siasa na uongozi",alisema.


Nae Mkurugenzi wa PEGAO Hafidh Abdi Said amesema mbali na juhudi zilizochukuliwa ila bado ushiriki wa wanawake  ni mdogo kwani hadi sasa kuna asilimia 38  ya viongozi wanawake.

" Kwenye asilimia hiyo wapo na wakuteuliwa, ni vyema  kuendelea kuhamasisha jamii ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kusimama na kusema wenyewe  na sio kuwasemea.

Wakitowa maoni yao miongoni mwa wahamasishaji jamii waliopata fursa ya kufikiwa na mradi huo Maryam Hemed Seif na  Omar Mjaka wamesema wapo tayari kuendelea kushirikiana na PEGAO katika kuhakikisha ushiriki wa wanawake kwenye ngazi za maamuzi unaongezeka.

"sisi kama wahamasishaji jamii ni vyema kujua wajibu wetu katika kuhamasisha wanawake kugombea katika ngazi za maamuzi kwani nao wanahaki kwa mujibu wa Katiba na sheria tofauti za nchi”,walisema.

SWIL ni mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki kwenye Demokrasia, Siasa na Uongozi unafadhiliwa na Ubalozi wa Norway na kutekelezwa na taasisi nne, ambazo ni Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania  @TAMWA_Zanzibar, Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba, @PEGAO,Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar @ZAFELA, Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar @JUWAUZA.  

Comments